PORT-OF-SPAIN, Trinidad na Tobago
VIONGOZI wa nchi wanachama wa Jumuia ya Madola wamekubali mpango wa kusaidia mataifa yanayoendelea kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, ikiwemo kupunguza gesi inayochafua mazingira.
Fedha hizo zilipendekezwa na viongozi wa Uingereza na Ufaransa katika mkutano huo uliomalizika mwishoni mwa wiki. Mpango huo utaanza mwakani kwa kutoa dola za Marekani bilioni 10 kila mwaka hadi itakapofika mwaka 2012.
Wanachama wengi wa Jumuia ya Madola ni mataifa ya visiwani ambayo yamekuwa katika tishio la kuongezeka kwa kina cha bahari.
Viongozi hao pia walitoa wito wa kutaka kufikia makubaliano yenye manufaa kwenye mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya hali ya hewa utakaofanyika mwezi ujao, Copenhagen, Denmark.
Waziri Mkuu wa Australia Kevin Rudd, alisema viongozi wa jumuia hiyo, wametafakari kuwa wakati wa kuchukua hatua kuhusu kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa ni sasa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki- Moon aliyehudhuria mkutano huo, alisema ana imani mkataba mpya kuhusu hali ya hewa utapatikana mjini Copenhagen.
Taarifa hiyo ya pamoja katika mkutano huo iliungwa mkono na nchi zote 53 wanachama wa Jumuia ya Madola.
Viongozi hao pia watawajibika kuhakikisha makubaliano yanaafikiwa kuhusu kupatikana kwa mkataba mpya ifikapo mwaka 2010, utakaoweka malengo ya kupunguzwa kwa utoaji wa gesi inayochafua mazingira.
Chanzo cha habari: Gazeti la Uhuru 30th Nov 2009








