Uhuru Publications Ltd - Gazeti Uhuru, Mzalendo na Burudani

Sunday
Sep 05th
Text size
  • Increase font size
  • Default font size
  • Decrease font size

Cirkovic kocha mpya Simba

E-mail Print PDF

NA DEUSDEDIT UNDOLE

WAKATI klabu ya Simba jana ilimtangaza rasmi Mserbia, Milovan Cirkovic kuwa kocha mpya wa timu hiyo, uongozi umemwangukia, Patrick Phiri ukimtaka kuandika barua ya kujiuzulu kabla ya kuanza Ligi Kuu

Tanzania Bara Agosti 21, mwaka huu. Kaimu Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala alisema wanatarajiwa kuingia mkataba wa miaka miwili na Cirkovic anayetarajiwa kuwasili nchini keshokutwa kuanza kazi. Cirkovic aliwahi kuinoa Simba kwa kipindi kifupi mwaka 2008 ambapo aliiongoza kwenda Abba kucheza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Enyimba ya Nigeria na kufungwa mabao 4-0 kabla ya kunyukwa mabao 3-1 katika mechi ya marudiano kwenye Uwanja wa Uhuru (zamani Taifa). "Katika kikao chetu tulifikia uamuzi wa kuingia mkataba wa miaka miwili na kocha raia wa Serbia, Milovan Cirkovic ili kwenda sambamba na maandalizi ya Simba inayojiandaa na Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa," alisema Mtawala. Katibu Mkuu huyo alisema kuwa Kamati ya Utendaji, iliamua kuchukua hatua hiyo baada ya Phiri kushindwa kutokea katika muda mwafaka kama walivyokubaliana na uongozi alipoondoka kwenda Zambia kwa mapumziko baada ligi kufikia ukingoni. Mtawala alidokeza kuwa kitendo cha Phiri kushindwa kurejea nchini mapema, kimechangia kuvuruga maandalizi ya Simba ambayo imepiga kambi Zanzibar kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Hisani kati yao na wapinzani wao Yanga uliopangwa kuchezwa Agosti 14, mwaka huu. "Simba ni zaidi ya kocha Phiri hatuwezi kukaa kimya tukisubiri mtu mmoja, hivyo kikao kimeamua kumsaka kocha mwingine ili aendelee na program za kukionoa kikosi hicho ambacho kwa sasa kimeweka kambi Zanzibar," alisema. Alisema uongozi umemwandia barua ya kumtaka ajiuzulu ili kutoa nafasi ya kocha mpya kuchukuwa nafasi yake na kuongeza kuwa wamefanya hivyo ili kulinda heshima ya Mzambia huyo ambaye kwa nyakati tofauti amewahi kuinoa Simba na kupata mafanikio. Mtawala alidai endapo wangechukuwa jukumu la kuandika barua ya kuvunja mkataba na Phiri uliobaki miezi mitatu, uongozi ungetakiwa kupeleka taarifa hizo Shirikisho la Soka Afrika (CAF) jambo alilodai siyo la kiungwana katika mchezo wa soka. Kabla ya kumtangaza Cirkovic, uongozi wa Simba ulimpa Phiri saa 24 ukimtaka kurejea nchini kuendelea na kazi. Timu hiyo imepiga kambi Zanzibar ikiwa chini ya kocha wa viungo Syllersaid Mziray na nahodha wa zamani wa kikosi hicho, Selemani Matola.

 

Magazeti Yetu

Habari za Kitaifa, Kimataifa, Uchumi, Biashara na Michezo kila siku

Habari za Kitaifa, Kimataifa, Uchumi, Biashara na Michezo kila Jumapili

Habari za Michezo, Tamthilia, Makala na Burudani kila Alhamisi

Toa Maoni Yako

Hali ya Kisiasa Tanzania