NA JOSEPH BURRA
KATIBU Mkuu wa CCM, Yussuf Makamba, amesema shahada ya mpiga kura iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) si kigezo cha kupiga kura za maoni keshokutwa. Makamba alisema hayo jana
alipozungumza na waandishi wa habari, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam, alipotoa maelekezo kwa viongozi wa Chama kuhusu upigaji kura za maoni. Amewaagiza viongozi wote wa CCM, hususan Kamati za Siasa za kila tawi kutowazuia wanachama halali kupiga kura za maoni kwa kigezo cha kutokuwa na shahada ya mpiga kura. Makamba alisema wanachama halali waliolipia robo au nusu ya ada ya mwaka waruhusiwe kupiga kura za maoni, kwa kuwa ni haki yao kikatiba kuchagua au kuchaguliwa. Awali, Chama kilielekeza wasiolipa ada ya mwaka na wasio na shahada ya mpiga kura wasipige kura hizo. "Katika uchaguzi wa mwaka huu hatutafanya kosa la kutoheshimu maoni ya wanachama, watakaopata kura nyingi ndio watakaopewa nafasi, tukikiuka hilo tutakuwa hatujitaki wenyewe," alisema Makamba. Kwa mujibu wa Makamba, matawi yatakuwa vituo vya kupigia kura na karatasi za kura zitakuwa na majina na picha halisi ya kila mgombea katika jimbo na kata husika. Katika hatua nyingine, Makamba aliipongeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kukamata baadhi ya wagombea ubunge na udiwani, akisema taasisi hiyo imeamka kufanya kazi zake. Alisema endapo itathibitika wagombea wanaochunguzwa na TAKUKURU wamehusika na rushwa, hawatateuliwa na Chama hata wakiwa na umaarufu unaofanana na Mlima Kilimanjaro, kwa kuwa rushwa ni kosa la jinai na inapigwa vita na Chama na serikali ya CCM. "Mwana-CCM akikamatwa kwa rushwa si jambo la kushangaza. Kwa ukubwa na umaarufu wa Chama, ningeshangaa kama matukio hayo yasingekuwepo. Tuna wanachama zaidi ya milioni tano, mbona Biblia imekataa watu wasizini lakini huzini, haya ni makosa ya mtu si ya Chama," alisema. Akisisitiza hilo, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Pius Msekwa, aliyehudhuria mkutano huo, alisema rushwa ni kosa la jinai sawa na ujambazi, hivyo jinai ielewe si katika siasa za CCM kama ambavyo wengi hutafsiri kuwa ni kawaida katika uchaguzi wa Chama. "Matukio ya rushwa ni makosa ya jinai, watakaokamatwa hushughulikiwa na vyombo vya dola, CCM hakina cha kufanya zaidi ya kukabidhi wanaotumumiwa katika vyombo husika na sheria kuchukua mkono wake," alisema Msekwa. Alisema vita dhidi ya rushwa si kazi ya CCM au mtu mmoja mmoja, bali ni jukumu la kila mtu katika jamii kujiepusha nalo, ili haki itendeke kwa kila mtu. Wakati huo huo, Makamba amemfananisha mgombea urais wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa na santuri mpya, ambayo huchezwa na kila mtu wakati inapotoka na baada ya wiki mbili hufifia umaarufu kwa watu kurejea santuri za awali. Kutokana na hilo, Makamba amewataka wana-CCM kutotishwa na ujio wa Dk. Slaa katika kinyang'anyiro cha urais mwaka huu, kwa kuwa umaarufu wake ni sawa na moto wa mabua, unaowaka kwa nguvu na kisha kuzimika ghafla bila kuacha kaa wala moshi baada ya muda mfupi.








