Na waandishi wetu Dar na mikoani
MBUNGE wa Arusha mjini, Felix Mrema, anayetetea nafasi hiyo, amekamatwa na kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa zaidi ya saa nane. Mrema alihojiwa usiku wa kuamkia jana, baada ya kukamatwa akituhumiwa kutoa rushwa kwa viongozi wa CCM tawi la Kiriki. Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Arusha, Ayoub Akida, alisema Mrema na watu wengine 20 walikamwa juzi, saa 4.30 usiku katika nyumba iliyopo eneo la Olomuriaki, kata ya Sombetini, Manispaa ya Arusha, wakipanga mikakati ya kumpatia ushindi. Alisema alipohojiwa Mrema alijitetea kuwa, yeye na timu yake walifika katika nyumba hiyo kumuona mgonjwa. Hata hivyo, Kamanda Akida alisema mgonjwa huyo hakuwepo, kwani hadi jana mchana alikuwa amelazwa Hospitali ya Mount Meru. Kamanda Akida alisema baada ya kupata maelezo hayo, walimwachia Mrema kwa dhamana saa 12 asubuhi kwa maelekezo iwapo atataka kusafiri nje ya mkoa anapaswa kutoa taarifa TAKUKURU. Alisema miongoni mwa waliokamatwa pamoja na Mrema ni kiongozi wa CCM wa tawi hilo, Shamsi Mwacha na mabalozi wa mashina yanayounda tawi hilo. Aliwataja mabalozi hao kuwa, Paulo Mollel, Jacob Mwita, Mama Sarah, Boniface Mweo, Siprian Mwamba na Abdala Gege, ambao pia waliachiwa kwa dhamana baada ya kuhojiwa. Wengine waliokamatwa ni Bakar Issa, Abdala Omar, Monika Nzota, Shaibu Waziri, Peter Ongiri, Asha Omar, Kolumba Mariri, Julius Lasizer, Alex Kisioki, Zuhura Shaaban, Waziri Kibune, Dixon Miambi, Elly Kileo na Fatuma Ally. Alisema walikutwa na sh. 115,000 zilizokuwa zimegawanywa mafungu matatu tofauti, zikiwa kwenye mkoba wa katibu wa tawi, kadi zaidi ya 20 za CCM, baadhi zikiwa hazina majina, ambazo zinahisiwa ni za kughushi. Kamanda Akida alisema wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo. Kuhusu wanandoa waliokamatwa juzi wakituhumiwa kutengeneza shahada bandia za kupigia kura nyumbani kwao, eneo la Sokon One, Manispaa ya Arusha, Kamanda Akida alisema bado wanawahoji. Alisema TAKUKURU inataka kufahamu watuhumiwa wanahusika na wagombea gani kati ya sita wanaowania kuteuliwa kupeperusha bendera ya Chama jimboni humo.
Mwakalinga chini ya ulinzi
WANANCHI wa kijiji cha Mababu, kata ya Matema, wilayani Kyela, wamemkamata mgombea ubunge, George Mwakalinga, kwa tuhuma za kukiuka maagizo waliyopewa na msimamizi wa uchaguzi, jimboni Kyela. Walichukua uamuzi huo kutokana na Mwakalinga kwenda kijijini humo saa tano usiku wakati msimamizi wa kampeni, Thabit Mzomozi, alisema ni marufuku mgombea kurudi kujieleza kwa wananchi baada ya kumaliza kampeni za pamoja. Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Mbeya, Respick Ndowo, alisema baada ya wananchi kuliona gari la Mwakalinga kijijini hapo, waliamua kumkamata na kutoa taarifa kwao. Ndowo alisema Mkuu wa TAKUKURU wilayani Kyela, Thomas Msuta, baada ya kupata taarifa hizo, alifika kijijini hapo saa 6.08 usiku na kukuta Mwakalinga, akiwa amewekwa chini ya ulinzi na baadhi ya wananchi. Alisema baada ya Msuta kuwauliza sababu ya kumuweka chini ya ulinzi Mwakalinga, walisema walikuwa wameelezwa na Mzomozi kuwa mgombea haruhusiwi kujieleza kwa wananchi baada ya kampeni za pamoja na wagombea wenzake, hivyo walimhoji amefuata nini kijijini hapo. “Mwakalinga aliwajibu hakwenda kufanya kampeni, bali alimfuata wakala wake, kwani muda wa kuonana naye ni mfupi kutokana na kutingwa na ratiba za kampeni,” alisema Ndowo. Kwa mujibu wa Ndowo, Msuta alimhoji Mwakalinga na kumpekua, baadae alilifanyia upekuzi gari lake lenye namba T 421 ADL, Toyota Land Cruiser, ambapo hakuna kilichopatikana kuashiria rushwa, zaidi ya sh. 11,500 alizokuwa nazo. Ndowo alisema TAKUKURU wilayani Kyela, inaendelea kulifanyia uchunguzi suala hilo ili kubaini ukweli na kuwataka wananchi kutojichukulia sheria mkononi, bali wanapokuwa na shaka watoe taarifa kwa vyombo husika. Wagombea wengine jimboni humo ni Mbunge anayemaliza muda wake, Dk. Harrison Mwakyembe, Rhoda Mwamunyange, Elius Mwakalinga na Elias Mwanjala. Katika hatua nyingine, mkutano wa kampeni uliokuwa ufanyike kata ya Ipinda haukufanyika, licha ya idadi kubwa ya wana-CCM kujitokeza. Ilidaiwa wagombea wote walikuwepo, lakini wasimamizi wa kampeni waliwachukua wagombea na kuondoka, huku wakiwaacha wanachama wakipigwa butwaa.
Wapambe wa Shigongo wanaswa
WAPAMBE wa mgombea ubunge Buchosa, Erick Shigongo, wametiwa mbaroni wakigawa fedha kwa wapiga kura katika kinyang’anyiro cha kura za maoni jimboni humo. Kamanda wa TAKUKURU mkoani Mwanza, Christopher Mariba, alisema jana kuwa wapambe hao walikamatwa juzi na maofisa wa taasisi hiyo, wakiwa na gari aina ya Nissan Patrol, ambalo hakutaja namba zake. Alisema taarifa kuwa, wapambe wawili wa mgombea huyo wanamwaga fedha kwa wanachama walizipata mapema na kuzifuatilia, ambapo juzi waliwatia mbaroni. “Baada ya kukamatwa walisema wanafanya biashara ya mpunga, lakini maelezo ya dereva na mtu mwingine aliyekuwa kwenye gari hilo yalitofautiana. Ndani ya gari kulikuwa na sh. 380,000, ambazo zote ni noti za sh. 1,000 na skafu za CCM,” alisema Kamanda Mariba. Alisema uchunguzi unaendelea na utakapokamilika hatua za kisheria zitachukuliwa.
Kimbisa ashushiwa shutuma
MEYA wa Jiji la Dar es Salaam, aliyemaliza muda wake, Adam Kimbisa, anayewania ubunge Dodoma Mjini, analalamikiwa na wagombea wengine 18 kuwa anawachafua katika kampeni zake. Wakizungumza kwa nyakati tofauti wagombea hao walidai hivi karibuni kupitia gazeti moja la kila siku (si Uhuru), Kimbisa alidai wagombea hao wanaburuzwa na mmoja wa wagombea. Katika taarifa hiyo, ilidaiwa mgombea Haidary Gulamali, anawaburuza wagombea wenzake kumpinga Kimbisa. Akizungumza na waandishi wa habari, Gulamali alikana kuwaburuza wenzake na kudai habari hizo si za kweli. Kwa mujibu wa Gulamali, anachojua ni kuwa Kimbisa hana ushirikiano na wenzake, hivyo amekuwa akijitenga. Mgombea Mohamed Morama, alidai Kimbisa amekuwa akiwachafua kwa kuwatolea lugha mbaya. Naye Amon Chaula, alidai mgombea huyo alimtolea maneno ya kashfa, na alimtaka kumuomba radhi, vinginevyo atamfikisha kwenye vyombo vya dola. Kimbasa hakupatikana kuzungumzia madai hayo.
Umri si kigezo -Kabisa
PETER Kabisa, anayewania ubunge Kinondoni, amesema umri si kigezo cha kutogombea nafasi hiyo. Kabisa alisema hayo jana katika ukumbi wa Lango la Jiji, alipojinadi kwa wanachama wa kata ya Mzimuni kutoka matawi ya Lango la Jiji, Makumbusho na Mtambani. Mwanachama wa kata hiyo, aliyejitambulisha Ramadhan, kutoka tawi la Lango la Jiji, alimuuliza Kabisa kuwa, umri wake umekwenda na alishaongoza jimbo hilo kwa miaka 10, kwa nini asipumzike ili awe mshauri wa vijana. Akijibu swali hilo, Kabisa akinukuu maeneo ya Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere alisema: “Wapeni vijana nafasi wanazoweza, lakini kama kuna wazee wanaoweza kwa nini muwaache?” Wagombea wengine ni Shy-Rose Bhanji, MackDonald Lunyilija, Nkurumah Munjoli, Kakolwa Mbano, Iddi Azzan, Mpoki Mwambulukutu, Mustapha Muro, Bakari Maige na Issa omary.








