NA KHADIJA MUSSA
BAADHI ya madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Hindu Mandal, Dar es Salaam, wanadaiwa kutoa taarifa za uongo kwamba mtoto aliyezaliwa amekufa, lakini muda mfupi baadae alibainika kuwa yu hai. Tukio hilo lililoacha maswali mengi lilitotokea juzi saa moja usiku, ambapo uongozi wa hospitali hiyo ulithibitisha kutokea, huku ukitia shaka juu ya mazingira yake. Habari zilizopatikana hospitalini hapo zilidai mjamzito aliyejifungua mtoto huyo alifikishwa hospitalini hapo kichanga hicho cha kiume kikiwa kimeanza kutoka. Ilidaiwa baada ya mjamzito huyo kusaidiwa na kumaliza kujifungua, alielezwa mwanawe amekufa, hivyo walikabidhiwa kichanga hicho kwa ajili ya maziko. Kwa mujibu wa chanzo cha habari, baada ya kufika nyumbani wakijiandaa na mazishi ya mtoto huyo, baba yake alipewa taarifa za kifo na aliomba asizikwe hadi atakapofika. Ilidaiwa baada ya baba huyo kufika nyumbani, mtoto huyo aliyekuwa amefunikwa nguo alipofunuliwa alionyesha dalili za kuwa hai, huku akijinyoosha, jambo lililowafanya wamrudishe hospitalini hapo. Chanzo hicho kilidai baada ya kufikishwa hospitalini, kichanga hicho kiliwekwa kwenye kifaa maalumu kinachotumika zaidi kwa watoto njiti. Imeelezwa kuwa kichanga hicho kilikaa katika kifaa hicho kwa saa tano, kabla daktari kueleza kuwa kimekufa. Habari zaidi zilidai baada ya uongozi wa hospitali kupata taarifa za kifo hicho, ulimrudishia mama mzazi sh. 400,000, fedha alizotoa kwa ajili ya huduma za kujifungua. Akizungumzia suala hilo jana, Dk. Kaushik Ramaiya, alisema walipata taarifa za tukio hilo juzi kutoka kwa daktari aliyekuwa zamu. Dk. Kaushik alisema mama huyo alifika hospitalini hapo akitokea hospitali ya Dar Group, akiwa katika hatua za mwisho za kujifungua. Alisema mama huyo alihudumiwa na daktari aliyemtaja kwa jina moja la Dk. Charles. "Baada ya mtoto kuzaliwa alionekana hana dalili za kuwa hai, wauguzi walitumia njia zote na walipothibitisha amefariki waliamua kumweleza mzazi kuwa mtoto amekufa. "Nilishangaa kusikia baba na shangazi wa mtoto huyo walisema walipofika nyumbani waliona mtoto anaanza kupumua na kumrudisha ambapo wauguzi walikiri anapumua na kumweka katika mashine,” alisema Dk. Kaushik. Hata hivyo, alisema tukio hilo ni la ajabu kwani halijawahi kutokea tangu aanze kazi ya udaktari miaka 29 iliyopita. Alisema wauguzi na daktari aliyekuwa zamu wakati wa tukio wametakiwa kutoa maelezo na kwamba uchunguzi unaendelea. Kuhusu mzazi kurudishiwa fedha, Dk. Kaushik alisema walifanya hivyo kwa ajili ya ubinadamu na si kwa nia nyingine yoyote.








